‏ 1 Samuel 5

Sanduku La Agano Huko Ashdodi Na Ekroni

1 aBaada ya Wafilisti kuteka Sanduku la Mungu, walilichukua kutoka Ebenezeri mpaka Ashdodi. 2 bKisha wakaliingiza lile Sanduku ndani ya hekalu la Dagoni na kuliweka kando ya huyo Dagoni. 3 cWatu wa Ashdodi walipoamka asubuhi na mapema kesho yake, kumbe, wakamkuta Dagoni ameanguka chini kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana! Wakamwinua Dagoni na kumrudisha mahali pake. 4 dLakini asubuhi iliyofuata, walipoamka kumbe, walimkuta huyo Dagoni ameanguka chini kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana! Kichwa chake na mikono vilikuwa vimevunjwa navyo vimelala kizingitini, ni kiwiliwili chake tu kilichokuwa kimebaki. 5 eNdiyo sababu mpaka leo makuhani wa Dagoni wala wengine waingiao katika hekalu la Dagoni huko Ashdodi hawakanyagi kizingiti.

6 fMkono wa Bwana ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi na vijiji jirani, akaleta uharibifu juu yao na kuwatesa kwa majipu. 7Watu wa Ashdodi walipoona kile kilichokuwa kikitokea, wakasema, “Sanduku la Mungu wa Israeli kamwe lisikae hapa pamoja na sisi, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya Dagoni mungu wetu.” 8 gBasi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kuwauliza, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Mungu wa Israeli?”

Wakajibu, “Sanduku la Mungu wa Israeli na liende Gathi.” Basi wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Israeli.

9 hLakini baada ya kulihamisha, mkono wa Bwana ulikuwa dhidi ya huo mji wa Gathi, akiuweka katika fadhaa kuu. Mungu akawatesa watu wa huo mji, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu. 10 iBasi wakapeleka Sanduku la Mungu Ekroni.

Wakati Sanduku la Mungu lilipokuwa linaingia Ekroni, watu wa Ekroni walilia wakisema “Wamelileta Sanduku la Mungu wa Israeli kwetu ili kutuua sisi na watu wetu.”
11Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kusema, “Liondoeni Sanduku la Mungu wa Israeli na lirudishwe mahali pake, la sivyo litatuua sisi na watu wetu.” Kwa kuwa kifo kilikuwa kimeujaza mji hofu; kwani mkono wa Mungu ulikuwa mzito sana juu yake. 12 jWale ambao hawakufa walipatwa na majipu, na kilio cha mji kilikwenda juu hadi mbinguni.

Copyright information for SwhNEN