2 Chronicles 30
Hezekia Aadhimisha Pasaka
1 aHezekia akatuma ujumbe kuwaita Israeli wote na Yuda, pia akaandika barua kwa Efraimu na Manase, kuwakaribisha ili waje hekaluni mwa Bwana huko Yerusalemu kuadhimisha Pasaka kwa Bwana, Mungu wa Israeli. 2 bMfalme na maafisa wake pamoja na kusanyiko lote katika Yerusalemu waliamua kuadhimisha Pasaka katika mwezi wa pili. 3 cKwa sababu makuhani hawakuwa wamejitakasa idadi ya kutosha na watu wakawa hawajakusanyika huko Yerusalemu, hawakuwa wameweza kuadhimisha Pasaka kwa wakati wake wa kawaida. 4Mpango huu ukaonekana wafaa kwa mfalme na kusanyiko lote. 5 dWakaamua kupeleka tangazo Israeli kote, kuanzia Beer-Sheba hadi Dani, wakiwaita watu waje Yerusalemu kuadhimisha Pasaka ya Bwana, Mungu wa Israeli. Ilikuwa haijaadhimishwa na idadi kubwa ya watu kama hiyo kufuatana na yale yaliyokuwa yameandikwa.6 eKwa amri ya mfalme, matarishi wakapita katika Israeli na Yuda kote wakiwa na barua kutoka kwa mfalme na kutoka kwa maafisa wake zikisema:
“Watu wa Israeli, mrudieni Bwana, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Israeli, ili naye awarudie ninyi mliosalia, mlionusurika kutoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru. 7 fMsiwe kama baba zenu na ndugu zenu, ambao hawakuwa waaminifu kwa Bwana, Mungu wa baba zao, hivyo akawafanya kitu cha kushangaza kama mnavyoona. 8 gMsiwe na shingo ngumu, kama baba zenu walivyokuwa, bali nyenyekeeni kwa Bwana. Njooni mahali patakatifu, alipopatakasa milele. Mtumikieni Bwana Mungu wenu, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nanyi. 9 hKama mkimrudia Bwana ndipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama ninyi mkimrudia yeye.”
10 iMatarishi wakaenda mji hadi mji katika Efraimu na Manase, wakafika mpaka Zabuloni, lakini watu wakawadharau na kuwadhihaki. 11 jLakini, baadhi ya watu wa Asheri, Manase na Zabuloni, wakajinyenyekeza wakaja Yerusalemu. 12 kPia katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa juu ya watu kuwapa umoja katika kutenda yale ambayo mfalme na maafisa wake waliwaamuru, kulingana na neno la Bwana.
13 lBasi umati mkubwa wa watu ukakusanyika huko Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu katika mwezi wa pili. 14 mWakajitia kazini kuyaondoa yale madhabahu yaliyokuwa huko Yerusalemu, wakayaondoa pia yale madhabahu ya kufukizia uvumba kwa miungu na kuyatupa Bonde la Kidroni.
15 nKisha wakamchinja mwana-kondoo wa Pasaka katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketezwa katika Hekalu la Bwana. 16 oKisha wakachukua nafasi zao za kawaida kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Mose mtu wa Mungu. Makuhani wakanyunyiza ile damu waliyokabidhiwa na Walawi. 17 pKwa kuwa wengi waliokuwa katika lile kusanyiko walikuwa hawajajitakasa, iliwapasa Walawi wachinje wana-kondoo wengine wa Pasaka kwa ajili ya wale watu ambao hawakuwa safi, kwa kufuata taratibu za ibada ili kuwatakasa kwa Bwana. 18 qIngawa watu wengi miongoni mwa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zabuloni walikuwa hawajajitakasa, hata hivyo walikula Pasaka kinyume na ilivyoandikwa. Lakini Hezekia akawaombea, akisema, “Bwana, ambaye ni mwema na amsamehe kila mmoja 19 rambaye anauelekeza moyo wake kumtafuta Mungu, Bwana, Mungu wa baba zake, hata kama yeye si safi kulingana na sheria za mahali patakatifu.” 20 sNaye Bwana akamsikia Hezekia akawaponya watu.
21 tWaisraeli waliokuwa Yerusalemu wakaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa muda wa siku saba, nao Walawi na makuhani walikuwa wakiimba kila siku, wakiwa na ala za uimbaji za kumsifu Bwana.
22 uHezekia akazungumza akiwatia moyo Walawi wote, ambao walionyesha ustadi katika kumtumikia Bwana. Hivyo watu wakala chakula cha sikukuu kwa siku saba, wakitoa sadaka za amani na kumshukuru Bwana, Mungu wa baba zao.
23 vKisha kusanyiko lote likakubali kuendelea na sikukuu kwa siku saba zaidi, kwa hiyo kwa siku saba nyingine wakaendelea kuiadhimisha kwa furaha. 24 wHezekia, mfalme wa Yuda akatoa mafahali 1,000, kondoo na mbuzi 7,000 kwa ajili ya kusanyiko, nao maafisa wakatoa mafahali 1,000 pamoja na kondoo na mbuzi 10,000. Idadi kubwa ya makuhani wakajiweka wakfu. 25 xKusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi na lile kusanyiko lote lililotoka Israeli, pamoja na wale wageni waliotoka Israeli na wale walioishi katika Yuda wakafurahi. 26Kulikuwa na furaha kubwa katika Yerusalemu, kwa sababu tangu siku za Mfalme Solomoni mwana wa Daudi mfalme wa Israeli halijakuwepo jambo kama hili katika Yerusalemu. 27 yNdipo makuhani na Walawi wakasimama wakawabariki watu, naye Mungu akawasikia, kwa sababu maombi yao yalifika mbinguni, makao yake matakatifu.
Copyright information for
SwhNEN