‏ 2 Peter 3

Ahadi Ya Kuja Kwa Bwana

1 aWapenzi, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa mawazo makamilifu. 2 bNataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa kupitia kwa mitume wenu.

3 cKwanza kabisa, ni lazima mfahamu ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka, wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbaya. 4 dWatasema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipofariki, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” 5 eLakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji. 6 fUlimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa. 7 gLakini kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.

8 hLakini wapenzi, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 iBwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.

10 jLakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.

11 kKwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12 lmkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. 13 mLakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.

14 nKwa sababu hii, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute katika amani, bila mawaa wala dosari. 15 oHesabuni uvumilivu wa Bwana kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu. 16 pHuandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote, akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha kwa maangamizi yao wenyewe, kama wapotoshavyo pia Maandiko mengine.

17 qBasi, ninyi wapenzi, kwa kuwa mmekwisha kujua mambo haya, jilindeni msije mkachukuliwa na kosa la watu hao waasi na kuanguka kutoka kwenye uthabiti wenu. 18 rBali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na milele! Amen.

Copyright information for SwhNEN