‏ 2 Samuel 1

Daudi Afahamishwa Kifo Cha Sauli

1 aBaada ya kifo cha Sauli, Daudi alipokuwa amerudi kutoka kuwashinda Waamaleki, Daudi alikaa siku mbili huko Siklagi. 2 bSiku ya tatu akaja mtu mwenye nguo zilizoraruka na mavumbi kichwani mwake kutoka kwenye kambi ya Sauli. Alipomjia Daudi, akajitupa chini ili kumpa heshima.

3Daudi akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?”

Akamjibu, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.”

4 cDaudi akamuuliza, “Ni nini kilichotokea? Niambie.”

Akasema, “Watu walikimbia kutoka vitani. Wengi wao walianguka na kufa. Naye Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa.”

5Ndipo Daudi akamwambia huyo kijana aliyemletea taarifa, “Je, umefahamuje kwamba Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?”

6 dYule kijana akasema, “Nilijipata huko Mlima Gilboa, naye Sauli alikuwa huko akiegemea mkuki wake, na magari ya vita na wapanda farasi wa upande wa adui wakawa wamemkaribia sana. 7Alipogeuka na kuniona, akaniita, nami nikasema, ‘Je, nifanye nini?’

8 e“Akaniuliza, ‘Wewe ni nani?’

“Nikamjibu, ‘Mimi ni Mwamaleki.’

9 f“Kisha akaniambia, ‘Nikaribie mimi na uniue! Niko katika maumivu makali ya kifo, lakini bado ningali hai.’

10 g“Kwa hiyo nikamkaribia nikamuua, kwa sababu nilijua kwamba baada ya kuanguka hangeweza kupona. Nami nikachukua lile taji lililokuwa kichwani mwake na utepe uliokuwa mkononi mwake nami nimevileta hapa kwa bwana wangu.”

11 hNdipo Daudi pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye wakazishika nguo zao na kuzirarua. 12Wakaomboleza, wakalia pia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Sauli na Yonathani mwanawe, kwa ajili ya jeshi la Bwana na nyumba ya Israeli, kwa sababu wameanguka kwa upanga.

13 iDaudi akamwambia yule kijana aliyemletea taarifa, “Wewe ni mwenyeji wa wapi?”

Akamjibu, “Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki.”

14 jDaudi akamuuliza, “Kwa nini hukuogopa kuinua mkono wako ili kumwangamiza mpakwa mafuta wa Bwana?”

15 kKisha Daudi akamwita mmoja wa watu wake na kumwambia, “Nenda ukamuue!” Kwa hiyo akampiga, naye akafa. 16 lKwa maana Daudi alikuwa amemwambia, “Damu yako iwe juu ya kichwa chako mwenyewe. Kinywa chako mwenyewe kimeshuhudia dhidi yako uliposema, ‘Nilimuua mpakwa mafuta wa Bwana.’ ”

Ombolezo La Daudi Kwa Ajili Ya Sauli Na Yonathani

17 mDaudi akafanya maombolezo haya kuhusu Sauli na Yonathani mwanawe, 18 nnaye akaagiza kwamba watu wa Yuda wafundishwe ombolezo hili la upinde (ambalo limeandikwa katika Kitabu cha Yashari):

19 o“Walio fahari yako, ee Israeli, wameuawa juu ya mahali pako palipoinuka.
Jinsi wenye nguvu walivyoanguka!

20 p“Msilisimulie hili katika Gathi,
msilitangaze hili katika
barabara za Ashkeloni,
binti za Wafilisti wasije wakafurahia,
binti za hao wasiotahiriwa
wasije wakashangilia.

21 q“Enyi milima ya Gilboa,
msipate umande wala mvua,
wala mashamba yazaayo sadaka ya nafaka.
Kwa maana huko ndiko ngao ya mwenye nguvu iliponajisiwa,
ngao ya Sauli haitapakwa tena mafuta.
22 rKutokana na damu ya waliouawa,
kutokana na miili ya wenye nguvu,
ule upinde wa Yonathani haukugeuka nyuma.
Upanga wa Sauli haukurudi bure.

23 s“Sauli na Yonathani,
maishani walipendwa na kuneemeka,
na katika kifo hawakutengana.
Walikuwa wepesi kuliko tai,
walikuwa na nguvu kuliko simba.

24 t“Enyi binti za Israeli,
lieni kwa ajili ya Sauli,
ambaye aliwavika nguo
nyekundu na maridadi,
ambaye aliremba mavazi yenu
kwa mapambo ya dhahabu.

25“Tazama jinsi mashujaa
walivyoanguka vitani!
Yonathani ameuawa
mahali pako palipoinuka.
26 uNahuzunika kwa ajili yako,
Yonathani ndugu yangu,
kwangu ulikuwa mpendwa sana.
Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu,
wa ajabu zaidi kuliko ule wa wanawake.

27 v“Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka!
Silaha za vita zimeangamia!”
Copyright information for SwhNEN