Daniel 2
Ndoto Ya Nebukadneza
1 aKatika mwaka wa pili wa utawala wake, Nebukadneza aliota ndoto. Mawazo yake yakasumbuka na hakuweza kulala. 2 bHivyo mfalme akawaita waganga, wasihiri, wachawi na wanajimu ili wamwambie ndoto yake aliyokuwa ameota. Walipoingia ndani na kusimama mbele ya mfalme, 3 cakawaambia, “Niliota ndoto inayonisumbua, nami nataka nijue maana yake.”4 dNdipo wanajimu wakamjibu mfalme kwa lugha ya Kiaramu, ▼ “Ee mfalme, uishi milele! Waambie watumishi wako hiyo ndoto, nasi tutaifasiri.”
5 fMfalme akawajibu wanajimu, “Nimeamua hivi kwa uthabiti: Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu ilikuwa ipi na kuifasiri, mtakatwa vipande vipande na nyumba zenu zitafanywa kuwa vifusi. 6 gLakini mkiniambia ndoto yangu na kuielezea, mtapokea kwangu zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi niambieni ndoto yangu na mnifasirie.”
7Wakajibu kwa mara nyingine, “Mfalme na awaambie watumishi wake ndoto yake, nasi tutaifasiri.”
8Ndipo mfalme akajibu, “Nina hakika kuwa mnajaribu kupata muda zaidi, kwa sababu mnatambua kuwa nimeamua hivi kwa uthabiti: 9 hIkiwa hamtaniambia ndoto yangu, ipo adhabu moja tu kwenu. Mmefanya shauri kuniambia habari za kunipotosha na mambo maovu, mkitumaini kwamba hali itabadilika. Hivyo basi, niambieni hiyo ndoto, nami nitajua kuwa mwaweza kunifasiria.”
10 iWanajimu wakamjibu mfalme, “Hakuna mtu duniani ambaye anaweza kufanya analotaka mfalme! Vilevile hakuna mfalme hata awe mkuu na mwenye uweza namna gani, aliyeuliza kitu kama hicho kwa mganga au kwa msihiri, wala kwa mnajimu yeyote. 11 jAnachouliza mfalme ni kigumu mno. Hakuna yeyote awezaye kumfunulia mfalme isipokuwa miungu, nao hawaishi miongoni mwa wanadamu.”
12 kJambo hili lilimkasirisha na kumghadhibisha mfalme mno hata kuagiza kuuawa kwa wenye hekima wote wa Babeli. 13 lHivyo amri ikatolewa ya kuwaua wenye hekima, nao watu wakatumwa kuwatafuta Danieli na rafiki zake ili wawaue.
14Wakati Arioko, mkuu wa askari wa walinzi wa mfalme, alikuwa amekwenda kuwaua watu wenye hekima wa Babeli, Danieli akazungumza naye kwa hekima na busara. 15Akamuuliza huyo afisa wa mfalme, “Kwa nini mfalme ametoa amri kali hivyo?” Ndipo Arioko akamweleza Danieli jambo hilo. 16Aliposikia jambo hili, Danieli akamwendea mfalme, akamwomba ampe muda ili aweze kumfasiria ile ndoto.
17Ndipo Danieli akarudi nyumbani kwake na kuwaeleza rafiki zake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo. 18 mAliwasihi waombe rehema kutoka kwa Mungu wa mbinguni kuhusu siri hii, ili yeye na rafiki zake wasije wakauawa pamoja na wenye hekima wengine wa Babeli. 19 nWakati wa usiku lile fumbo lilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Ndipo Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni, 20 ona akasema:
“Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele;
hekima na uweza ni vyake.
21 pYeye hubadili nyakati na majira;
huwaweka wafalme na kuwaondoa.
Huwapa hekima wenye hekima,
na maarifa wenye ufahamu.
22 qHufunua siri na mambo yaliyofichika;
anajua yale yaliyo gizani,
nayo nuru hukaa kwake.
23 rNinakushukuru na kukuhimidi,
Ee Mungu wa baba zangu:
Umenipa hekima na uwezo,
umenijulisha kile tulichokuomba,
umetujulisha ndoto ya mfalme.”
Danieli Aifasiri Ndoto
24 sNdipo Danieli akamwendea Arioko, ambaye mfalme alikuwa amemteua kuwaua wenye hekima wa Babeli, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babeli. Nipeleke kwa mfalme, nami nitamfasiria ndoto yake.”25 tArioko akampeleka Danieli kwa mfalme mara moja na kumwambia, “Nimempata mtu miongoni mwa watu wa uhamisho kutoka Yuda ambaye anaweza kumwambia mfalme maana ya ndoto yake.”
26 uMfalme akamuuliza Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza), “Je, unaweza kuniambia nilichoona katika ndoto yangu na kuifasiri?”
27 vDanieli akajibu, “Hakuna mwenye hekima, msihiri, mganga au mwaguzi anayeweza kumweleza mfalme siri aliyouliza, 28 wlakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri. Amemwonyesha Mfalme Nebukadneza kitakachotokea siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyopita mawazoni mwako ulipokuwa umelala kitandani mwako ni haya:
29“Ee mfalme, ulipokuwa umelala kitandani, yalikujia mawazo kuhusu mambo yatakayotokea baadaye, naye mfunuaji wa siri akakuonyesha ni kitu gani kitakachotokea. 30 xKwangu mimi, nimefunuliwa siri hii, si kwa sababu nina hekima kubwa kuliko watu wengine wanaoishi, bali ni ili wewe, ee mfalme, upate kujua tafsiri, na ili uweze kuelewa kile kilichopita mawazoni mwako.
31 y“Ee mfalme, ulitazama, na mbele yako ilisimama sanamu kubwa, kubwa mno kupita kiasi, sanamu iliyongʼaa na kutisha kwa kuonekana kwake. 32Kichwa cha ile sanamu kilikuwa kimetengenezwa kwa dhahabu safi, kifua chake na mikono yake vilikuwa vya fedha, tumbo lake na mapaja yake vilikuwa vya shaba, 33miguu yake ilikuwa ya chuma, na nyayo zake zilikuwa chuma nazo sehemu nyingine zilikuwa udongo wa mfinyanzi uliochomwa. 34 zUlipokuwa unaangalia, jiwe lilikatwa, lakini si kwa mikono ya mwanadamu. Lile jiwe liliipiga ile sanamu kwenye nyayo zake za chuma na udongo wa mfinyanzi, na kuivunja. 35 aaNdipo ile chuma, ule udongo wa mfinyanzi, ile shaba, ile fedha na ile dhahabu vikavunjika vipande vipande kwa wakati mmoja, na vikawa kama makapi katika sakafu ya kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperusha bila kuacha hata alama. Lakini lile jiwe lililoipiga ile sanamu likawa mlima mkubwa mno na kuijaza dunia yote.
36 ab“Hii ndiyo iliyokuwa ndoto, nasi sasa tutamfasiria mfalme. 37 acEe mfalme, wewe ni mfalme wa wafalme. Mungu wa mbinguni amekupa wewe utawala, uweza, nguvu na utukufu. 38 adMikononi mwako amewaweka wanadamu, wanyama wa kondeni, na ndege wa angani. Popote waishipo amekufanya wewe kuwa mtawala juu yao wote. Wewe ndiye kile kichwa cha dhahabu.
39 ae“Baada yako, ufalme mwingine utainuka, ulio dhaifu kuliko wako. Baadaye utafuata ufalme wa tatu, ule wa shaba, nao utatawala juu ya dunia yote. 40 af , agHatimaye, kutakuwako na ufalme wa nne, wenye nguvu kama chuma, kwa maana chuma huvunja na kupondaponda kila kitu; kama vile chuma ivunjavyo vitu vipande vipande, ndivyo ufalme huo utakavyopondaponda na kuvunjavunja nyingine zote. 41Kama vile ulivyoona kuwa kwa sehemu nyayo na vidole vilikuwa vya udongo wa mfinyanzi uliochomwa na kwa sehemu nyingine chuma, hivyo huu utakuwa ufalme uliogawanyika; hata hivyo utakuwa na sehemu zenye nguvu za chuma ndani yake, kama vile ulivyoona chuma imechanganywa na udongo wa mfinyanzi. 42Kama vile vidole vyake vya miguu vilikuwa kwa sehemu chuma na sehemu udongo wa mfinyanzi, hivyo ufalme huo kwa sehemu utakuwa na nguvu na kwa sehemu udhaifu. 43Kama vile ulivyoona chuma kikiwa kimechanganyikana na udongo wa mfinyanzi uliochomwa, ndivyo watu watakavyokuwa mchanganyiko, wala hawatabaki wameungana tena, kama vile chuma kisivyoweza kuchanganyikana na udongo wa mfinyanzi.
44 ah“Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atauweka ufalme ambao kamwe hautaangamizwa, wala hautaachiwa taifa jingine. Utaziponda zile falme zote na kuzikomesha, bali wenyewe utadumu milele. 45 aiHii ndiyo maana ya maono ya jiwe lililochongwa kutoka mlimani, lakini si kwa mikono ya mwanadamu, lile jiwe ambalo lilivunja chuma, shaba, udongo wa mfinyanzi, fedha na dhahabu vipande vipande.
“Mungu Mkuu amemwonyesha mfalme kile kitakachotokea wakati ujao. Ndoto hii ni ya kweli na tafsiri yake ni ya kuaminika.”
46 ajNdipo Mfalme Nebukadneza akaanguka kifudifudi mbele ya Danieli kumpa heshima, akaagiza wamtolee Danieli sadaka na uvumba. 47 akMfalme akamwambia Danieli, “Hakika Mungu wako ni Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, na mfunuaji wa siri zote, kwa maana umeweza kufunua siri hii.”
48 alNdipo mfalme akamweka Danieli nafasi ya juu, na kumpa zawadi nyingi tele. Akamfanya kuwa mtawala wa jimbo lote la Babeli, na kumweka kuwa mkuu wa wenye hekima wote. 49 amZaidi ya hayo, kwa ombi la Danieli, mfalme akawateua Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa wasimamizi wa jimbo la Babeli, huku Danieli akibaki katika ukumbi wa mfalme.
Copyright information for
SwhNEN