Ecclesiastes 4
Uonevu, Taabu, Uadui
1 aNikatazama tena nikaona uonevu wote uliokuwa unafanyika chini ya jua:Nikaona machozi ya walioonewa,
wala hawana wa kuwafariji;
uwezo ulikuwa upande wa wale wanaowaonea,
wala hawana wa kuwafariji.
2 bNami nikasema kwamba wafu,
waliokwisha kufa,
wana furaha kuliko watu walio hai,
ambao bado wanaishi.
3 cLakini aliye bora kuliko hao wawili
ni yule ambaye hajazaliwa bado,
ambaye hajaona ule uovu
unaofanyika chini ya jua.
4Tena nikaona kuwa kazi zote na mafanikio yote huchipuka kutokana na wivu wa mtu kwa jirani yake. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
5 dMpumbavu hukunja mikono yake
na kujiangamiza mwenyewe.
6 eAfadhali konzi moja pamoja
na utulivu kuliko konzi mbili pamoja na taabu
na kukimbiza upepo.
7Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua:
8 fKulikuwepo mwanadamu aliye peke yake,
hakuwa na mwana wala ndugu.
Hapakuwa na mwisho wa kazi yake,
hata hivyo macho yake
hayakutosheka na utajiri wake.
Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani,
nami kwa nini ninajinyima kufurahia?”
Hili pia ni ubatili,
ni shughuli yenye taabu!
9Wawili ni afadhali kuliko mmoja,
kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao:
10Kama mmoja akianguka,
mwenzake atamwinua.
Lakini ni jambo la kuhuzunisha
kwa mtu yule aangukaye
naye hana wa kumwinua!
11Pia, kama wawili wakilala pamoja
watapashana joto.
Lakini ni vipi mtu aweza
kujipasha joto mwenyewe?
12Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa,
watu wawili wanaweza
kumkabili adui na kumshinda.
Kamba ya nyuzi tatu
haikatiki kwa urahisi.
Maendeleo Ni Ubatili
13Afadhali kijana maskini mwenye hekima kuliko mfalme mzee mpumbavu ambaye hajui tena kupokea maonyo. 14Kijana huyo angeweza kutokea gerezani akapata ufalme, au angeweza kuwa amezaliwa katika umaskini kwenye huo ufalme. 15Nikaona kwamba wote walioishi na kutembea chini ya jua walimfuata kijana, aliyepokea ufalme. 16Hapakuwa na kikomo cha watu wote aliowatawala. Lakini wale waliokuja baadaye hawakufurahia kazi ya yule aliyepokea ufalme. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
Copyright information for
SwhNEN