Genesis 27
Yakobo Anaipata Baraka Ya Isaki
1Isaki alipokuwa mzee na macho yake yalipokuwa yamekosa nguvu asiweze kuona tena, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.”Akajibu, “Mimi hapa.”
2Isaki akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kifo changu. 3 aSasa basi, chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukawinde nyama pori kwa ajili yangu. 4Uniandalie aina ya chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili niweze kukubariki kabla sijafa.”
5Basi Rebeka alikuwa akisikiliza Isaki alipokuwa akizungumza na mwanawe Esau. Esau alipoondoka kwenda nyikani kuwinda nyama pori na kuleta, 6Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau, 7‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili niweze kukubariki mbele za Bwana kabla sijafa.’ 8 bSasa, mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia: 9Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili niandalie chakula kitamu kwa ajili ya baba yako, kama vile anavyopenda. 10Kisha umpelekee baba yako ale, ili apate kukubariki kabla hajafa.”
11 cYakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Lakini ndugu yangu Esau ana nywele mwilini, mimi nina ngozi nyororo. 12 dItakuwaje kama baba yangu akinigusa? Itaonekana kwake kama niliyemfanyia ujanja na kuleta laana juu yangu badala ya baraka.”
13Mama yake akamwambia, “Mwanangu, laana na iwe juu yangu. Fanya tu ninalokuambia, nenda ukaniletee hao wana-mbuzi.”
14Kwa hiyo alikwenda akawaleta, akampa mama yake, akaandaa chakula kitamu, kama vile alivyopenda baba yake. 15 eKisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. 16Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi. 17Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka.
18Akamwendea baba yake akasema, “Baba yangu.”
Akajibu, “Naam, mwanangu, wewe ni nani?”
19 fYakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniambia. Tafadhali uketi, ule sehemu ya mawindo yangu ili uweze kunibariki.”
20Isaki akamuuliza mwanawe. “Umepataje haraka namna hii, mwanangu?”
Akajibu, “Bwana Mungu wako amenifanikisha.”
21 gKisha Isaki akamwambia Yakobo, “Mwanangu tafadhali sogea karibu nami ili nikupapase, nione kama hakika ndiwe Esau mwanangu, au la.”
22Yakobo akasogea karibu na baba yake Isaki, ambaye alimpapasa na kusema, “Sauti ni ya Yakobo, bali mikono ni ya Esau.” 23 hHakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na nywele kama ya ndugu yake Esau, kwa hiyo akambariki. 24Akamuuliza, “Hivi kweli wewe ni mwanangu Esau?”
Akajibu, “Mimi ndiye.”
25 iKisha akasema, “Mwanangu, niletee sehemu ya mawindo yako nile, ili nipate kukubariki.”
Yakobo akamletea naye akala, akamletea na divai akanywa. 26Kisha Isaki baba yake akamwambia, “Njoo hapa, mwanangu, unibusu.”
27 jKwa hiyo akamwendea akambusu. Isaki aliposikia harufu ya nguo zake, akambariki, akasema,
“Aha, harufu ya mwanangu
ni kama harufu ya shamba
ambalo Bwana amelibariki.
28 kMungu na akupe umande kutoka mbinguni
na utajiri wa duniani:
wingi wa nafaka na divai mpya.
29 lMataifa na yakutumikie
na mataifa yakusujudie.
Uwe bwana juu ya ndugu zako,
na wana wa mama yako wakusujudie.
Walaaniwe wale wakulaanio,
nao wale wakubarikio wabarikiwe.”
30 mBaada ya Isaki kumaliza kumbariki na baada tu ya Yakobo kuondoka kwa baba yake, ndugu yake Esau akaingia kutoka mawindoni. 31 nNaye pia akaandaa chakula kitamu akamletea baba yake. Kisha akamwambia, “Baba yangu, keti ule sehemu ya mawindo yangu, ili upate kunibariki.”
32 oIsaki baba yake akamuuliza, “Wewe ni nani?”
Akajibu, “Mimi ni mwanao, mzaliwa wako wa kwanza, Esau.”
33 pIsaki akatetemeka kwa nguvu sana, akasema, “Alikuwa nani basi, ambaye aliwinda mawindo akaniletea? Nilikula kabla tu hujaja na nikambariki, naye hakika atabarikiwa!”
34 qEsau aliposikia maneno haya ya baba yake, akalia sauti kubwa na ya uchungu, na kumwambia baba yake, “Nibariki mimi, mimi pia, baba yangu!”
35 rLakini akasema, “Ndugu yako amekuja kwa udanganyifu na akachukua baraka yako.”
36 sEsau akasema, “Si ndiyo sababu anaitwa Yakobo? Amenidanganya mara hizi mbili: Alichukua haki yangu ya kuzaliwa na sasa amechukua baraka yangu!” Kisha akauliza, “Hukubakiza hata baraka moja kwa ajili yangu?”
37 tIsaki akamjibu Esau, “Nimemfanya yeye kuwa bwana juu yako, pia nimewafanya ndugu zako wote kuwa watumishi wake, nimemtegemeza kwa nafaka na divai mpya. Sasa nitaweza kukufanyia nini, mwanangu?”
38 uEsau akamwambia baba yake, “Je, baba yangu una baraka moja tu? Unibariki mimi pia, baba yangu!” Kisha Esau akalia kwa sauti kubwa.
39 vBaba yake Isaki akamjibu, akamwambia,
“Makao yako yatakuwa
mbali na utajiri wa dunia,
mbali na umande wa mbinguni juu.
40 wUtaishi kwa upanga,
nawe utamtumikia ndugu yako,
lakini wakati utakapokuwa umejikomboa,
utatupa nira yake
kutoka shingoni mwako.”
Yakobo Anakimbilia Kwa Labani
41 xEsau akawa na kinyongo dhidi ya Yakobo kwa ajili ya baraka ambazo baba yake alikuwa amembariki. Akasema moyoni mwake, “Siku za kuomboleza kwa ajili ya baba yangu zimekaribia, ndipo nitamuua ndugu yangu Yakobo.”42Rebeka alipokwisha kuambiwa yale aliyoyasema Esau mwanawe mkubwa, alimwita Yakobo mwanawe mdogo, akamwambia, “Ndugu yako Esau anajifariji kwa wazo la kukuua. 43 ySasa basi, mwanangu, fanya nisemalo: Kimbilia haraka kwa Labani ndugu yangu kule Harani. 44Ukae naye kwa muda mpaka ghadhabu ya ndugu yako itulie. 45 zWakati ndugu yako atakapokuwa hana hasira nawe tena na amesahau uliyomtendea, nitakupelekea ujumbe urudi. Kwa nini niwapoteze wote wawili kwa siku moja?”
46 aaKisha Rebeka akamwambia Isaki, “Nimechukia kuishi kwa sababu ya hawa wanawake wa Kihiti. Ikiwa Yakobo ataoa mke miongoni mwa wanawake wa nchi hii, wanawake wa Kihiti kama hawa, sitakuwa na faida kuendelea kuishi.”
Copyright information for
SwhNEN