Job 41
1 a“Je, waweza kumvua Lewiathani ▼▼Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa.
kwa ndoano ya samaki,au kufunga ulimi wake kwa kamba?
2 cWaweza kupitisha kamba puani mwake,
au kutoboa taya lake kwa kulabu?
3 dJe, ataendelea kukuomba umhurumie?
Atasema nawe maneno ya upole?
4 eJe, atafanya agano nawe ili umtwae
awe mtumishi wako maisha yake yote?
5Je, utamfuga na kumfanya rafiki kama ndege,
au kumfunga kamba kwa ajili ya wasichana wako?
6Je, wafanyabiashara watabadilishana bidhaa kwa ajili yake?
Watamgawanya miongoni mwa wafanyao biashara?
7 fJe, waweza kuijaza ngozi yake kwa vyuma vyenye ncha kali,
au kichwa chake kwa mkuki wa kuvulia samaki?
8 gKama ukiweka mkono wako juu yake,
utavikumbuka hivyo vita na kamwe hutarudia tena!
9 hTumaini lolote la kumtiisha ni kujidanganya;
kule kumwona tu kunamwangusha mtu chini.
10 iHakuna yeyote aliye mkali athubutuye kumchokoza.
Ni nani basi awezaye kusimama dhidi yangu?
11 jNi nani mwenye madai dhidi yangu ili nipate kumlipa?
Kila kitu kilicho chini ya mbingu ni mali yangu.
12 k“Sitashindwa kunena juu ya maungo yake,
nguvu zake na umbo lake zuri.
13 lNi nani awezaye kumvua gamba lake la nje?
Ni nani awezaye kumsogelea na lijamu?
14 mNani athubutuye kuufungua mlango wa kinywa chake,
kilichozungukwa na meno yake ya kutisha pande zote?
15 nMgongo wake una safu za ngao
zilizoshikamanishwa imara pamoja;
16kila moja iko karibu sana na mwenzake,
wala hakuna hewa iwezayo kupita kati yake.
17Zimeunganishwa imara kila moja na nyingine;
zimengʼangʼaniana pamoja wala haziwezi kutenganishwa.
18 oAkipiga chafya mwanga humetameta;
macho yake ni kama mionzi ya mapambazuko.
19 pMienge iwakayo humiminika kutoka kinywani mwake;
cheche za moto huruka nje.
20 qMoshi hufuka kutoka puani mwake,
kama kutoka kwenye chungu kinachotokota kwa moto wa matete.
21 rPumzi yake huwasha makaa ya mawe,
nayo miali ya moto huruka kutoka kinywani mwake.
22 sNguvu hukaa katika shingo yake;
utisho hutangulia mbele yake.
23Mikunjo ya nyama yake imeshikamana imara pamoja;
iko imara na haiwezi kuondolewa.
24 tKifua chake ni kigumu kama mwamba,
kigumu kama jiwe la chini la kusagia.
25 uAinukapo, mashujaa wanaogopa;
hurudi nyuma mbele yake anapokwenda kwa kishindo.
26 vUpanga unaomfikia haumdhuru,
wala mkuki au mshale wala fumo.
27 wChuma hukiona kama unyasi,
na shaba kama mti uliooza.
28 xMishale haimfanyi yeye akimbie;
mawe ya kombeo kwake ni kama makapi.
29 yRungu kwake huwa kama kipande cha jani kavu;
hucheka sauti za kugongana kwa mkuki.
30 zSehemu zake za chini kwenye tumbo
zina menomeno na mapengo kama vigae vya chungu,
zikiacha mburuzo kwenye matope
kama chombo chenye meno cha kupuria.
31 aaHuvisukasuka vilindi kama sufuria kubwa ichemkayo,
na kukoroga bahari kama chungu cha marhamu.
32Anapopita nyuma yake huacha mkondo unaometameta;
mtu angedhani vilindi vilikuwa na mvi.
33 abHakuna chochote duniani kinacholingana naye:
yeye ni kiumbe kisicho na woga.
34 acYeye huwatazama chini wale wote wenye kujivuna;
yeye ni mfalme juu ya wote wenye kiburi.”
Copyright information for
SwhNEN