‏ John 20

Kufufuka Kwa Yesu

(Mathayo 28:1-8; Marko 16:1-8; Luka 24:1-12)

1 aAlfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa kungali giza bado, Maria Magdalene alikwenda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio. 2 bHivyo akaja akikimbia kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, na kusema, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na hatujui walikomweka!”

3 cPetro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara kuelekea kaburini. 4Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. 5 dAlipofika, akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani mle ndani, lakini hakuingia. 6Ndipo Simoni Petro akaja, akimfuata nyuma akaenda moja kwa moja hadi ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini 7 ena kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Yesu. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa mahali pa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda. 8 fKisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini naye akaingia ndani, akaona, akaamini, 9 g(kwa kuwa mpaka wakati huo walikuwa bado hawajaelewa kutoka Maandiko kwamba ilikuwa lazima Yesu afufuke kutoka kwa wafu).

10Kisha hao wanafunzi wakaondoka wakarudi nyumbani kwao.

Yesu Anamtokea Maria Magdalene

(Mathayo 28:9-10; Marko 16:9-11)

11 hLakini Maria Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama, kuchungulia mle kaburini, 12 inaye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.

13 jWakamuuliza Maria, “Mwanamke, mbona unalia?”

Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu na sijui walikomweka.”
14 kBaada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Yesu amesimama, lakini hakumtambua.

15 lYesu akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?”

Maria akidhani ya kuwa aliyekuwa anaongea naye ni mtunza bustani, kwa hiyo akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nionyeshe ulikomweka, nami nitamchukua.”

16 mYesu akamwita, “Maria!”

Ndipo Maria akamgeukia Yesu na kusema naye kwa Kiebrania, “Rabboni!” (maana yake Mwalimu).

17 nYesu akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ”

18 oKwa hiyo Maria Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Yesu, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Yesu alikuwa amemweleza mambo hayo yote.

Yesu Awatokea Wanafunzi Wake

(Mathayo 28:16-20; Marko 16:14-18; Luka 24:36-49)

19Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi. Naye Yesu aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” 20 pBaada ya kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana.

21 qYesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” 22 rNaye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23 sMkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa, na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.”

Yesu Anamtokea Tomaso

24 tLakini Tomaso, aliyeitwa Didimasi, yaani Pacha, mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Yesu alipokuja. 25 uHivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.”

Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake, na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.”

26 vBaada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomaso alikuwa pamoja nao. Ndipo Yesu akaja milango ikiwa imefungwa na kusimama katikati yao akasema, “Amani iwe nanyi.” 27 wKisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyoosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.”

28 xTomaso akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”

29 yYesu akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”

Kusudi La Kitabu Hiki

30 zYesu alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki. 31 aaLakini haya yameandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Yesu ndiye Kristo,
Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.

Copyright information for SwhNEN