‏ Titus 3

Kutenda Mema

1 aWakumbushe watu kuwanyenyekea watawala na kuwatii wenye mamlaka, wawe tayari kutenda kila lililo jema. 2 bWasimnenee mtu yeyote mabaya, wasiwe wagomvi, bali wawe wapole, wakionyesha unyenyekevu kwa watu wote.

3 cMaana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi. 4 dLakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa, 5 ealituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kwa njia ya Roho Mtakatifu, 6 fambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu, 7 gili kwamba, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele. 8 hHili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu.

9 iLakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu hayana faida, tena ni ubatili. 10 jMtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena. 11 kKwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.

Maneno Ya Mwisho Na Kumtamkia Baraka

12 lMara nitakapomtuma Artema au Tikiko kwako, jitahidi kuja unione huko Nikopoli, kwa sababu nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi. 13 mFanya kila uwezalo uwasafirishe Zena yule mwanasheria na Apolo na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji katika safari yao. 14Watu wetu hawana budi kujifunza kutenda mema, ili waweze kuyakimu mahitaji ya kila siku, wasije wakaishi maisha yasiyokuwa na matunda.

15 nWote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu wale wanaotupenda katika imani.

Neema iwe nanyi nyote. Amen.

Copyright information for SwhNEN