‏ 1 Corinthians 13

Karama Ya Upendo

1 aHata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo. 2 bNingekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. 3 cKama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.

4 dUpendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 eHaukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 fUpendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 gUpendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.

8 hUpendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita. 9 iKwa maana tunafahamu kwa sehemu na tunatoa unabii kwa sehemu. 10 jLakini ukamilifu ukija, yale yasiyo kamili hutoweka. 11 kNilipokuwa mtoto, nilisema kama mtoto, niliwaza kama mtoto, nilifikiri kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima niliacha mambo ya kitoto. 12 lKwa maana sasa tunaona taswira kama kwa kioo, lakini wakati huo tutaona wazi. Sasa nafahamu kwa sehemu, wakati huo nitafahamu kikamilifu, kama vile mimi ninavyofahamika kikamilifu.

13 mBasi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.

Copyright information for SwhNEN