‏ 2 Kings 17:28-41

28Basi mmoja wa makuhani ambaye alikuwa amepelekwa uhamishoni kutoka Samaria akaja kuishi Betheli na kuwafundisha jinsi ya kumwabudu Bwana.

29 aHata hivyo, kila kikundi cha taifa lililoletwa Samaria kilitengeneza miungu yao wenyewe katika miji kadhaa mahali walipoishi, nao wakaiweka mahali pa ibada za miungu ambapo watu wa Samaria walikuwa wametengeneza katika mahali pa juu. 30Watu kutoka Babeli wakamtengeneza Sukoth-Benothi kuwa mungu wao, watu kutoka Kutha wakamtengeneza Nergali, na watu kutoka Hamathi wakamtengeneza Ashima; 31 bWaavi wakatengeneza Nibhazi na Tartaki, nao Wasefarvi wakachoma watoto wao kama kafara kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. 32 cWalimwabudu Bwana, lakini pia waliteua aina zote za watu wao ili kuwawakilisha kama makuhani katika mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu pa ibada. 33Walimwabudu Bwana, lakini pia waliitumikia miungu yao kulingana na desturi za mataifa walikotoka.

34 dMpaka leo wanashikilia desturi zao za zamani. Hawamwabudu Bwana wala kuzishika hukumu na maagizo, sheria na amri ambazo Bwana aliwapa uzao wa Yakobo, ambaye alimwita Israeli. 35 eWakati Bwana alipofanya Agano na Waisraeli, aliwaamuru akisema: “Msiiabudu miungu mingine yoyote wala kuisujudia, wala kuitumikia wala kuitolea dhabihu. 36 fBali imewapasa kumwabudu Bwana aliyewapandisha kutoka Misri kwa uwezo wake mkuu na kwa mkono wake ulionyooshwa. Kwake yeye mtasujudu na kwake yeye mtatoa dhabihu. 37 gImewapasa daima kuwa waangalifu kutunza hukumu na maagizo, sheria na amri alizowaandikia. Msiabudu miungu mingine. 38 hMsisahau agano nililofanya nanyi, wala msiabudu miungu mingine. 39Bali, mtamwabudu Bwana Mungu wenu, kwani yeye ndiye atakayewakomboa kutoka mikononi mwa adui zenu wote.”

40Hata hivyo hawakusikiliza, lakini waliendelea na desturi zao za awali. 41 iHata wakati watu hawa walipokuwa wanamwabudu Bwana, walikuwa bado wakitumikia sanamu zao. Mpaka leo watoto wao na watoto wa watoto wao wanaendelea kufanya kama baba zao walivyofanya.

Copyright information for SwhNEN