‏ 2 Kings 21:3-15

3 aAkajenga upya mahali pa juu pa kuabudia miungu ambapo Hezekia baba yake alikuwa amepabomoa. Pia akasimamisha madhabahu za Baali na kutengeneza nguzo ya Ashera, kama Ahabu mfalme wa Israeli alivyofanya. Akalisujudia jeshi lote la angani na kuliabudu. 4 bAkajenga madhabahu katika Hekalu la Bwana, ambamo Bwana alikuwa amesema, “Katika Yerusalemu nitaliweka Jina langu.” 5 cKatika nyua zote mbili za Hekalu la Bwana, akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani. 6 dAkamtoa kafara mwanawe mwenyewe katika moto, akafanya uchawi na uaguzi, na akataka shauri kwa wapiga ramli na kwa mizimu. Akafanya maovu mengi sana machoni mwa Bwana na kumghadhibisha.

7 eAkachukua nguzo ya Ashera aliyoichonga na kuiweka katika Hekalu, ambalo Bwana alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Solomoni, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu niliouchagua kutoka kabila zote za Israeli, nitaliweka Jina langu milele. 8 fSitaifanya tena miguu ya Waisraeli itangetange kutoka nchi niliyowapa baba zao, ikiwa watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru, na kuishika Sheria yote ambayo walipewa na Mose mtumishi wangu.” 9 gLakini hawa watu hawakusikiliza. Manase akawapotosha, hivyo kwamba walifanya maovu mengi kuliko mataifa ambayo Bwana aliyaangamiza mbele ya Waisraeli.

10 Bwana akasema kupitia watumishi wake manabii: 11 h“Manase mfalme wa Yuda ametenda dhambi hizi za kuchukiza. Amefanya maovu mengi kuliko Waamori waliokuwepo kabla yake, na ameiongoza Yuda katika dhambi kwa sanamu zake. 12 iKwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nitaleta maafa makubwa juu ya Yerusalemu na Yuda, kiasi kwamba masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yatawasha. 13 jNitanyoosha juu ya Yerusalemu kamba ya kupimia iliyotumika dhidi ya Samaria, na timazi iliyotumika dhidi ya nyumba ya Ahabu. Nitaifutilia mbali Yerusalemu kama mtu afutaye sahani, nikiifuta na kuifunikiza. 14 kNitawakataa mabaki wa urithi wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao. Watapokonywa mali zao na kutekwa nyara na adui zao wote, 15 lkwa sababu wametenda uovu machoni pangu na kunighadhibisha tangu siku baba zao walipotoka Misri mpaka siku ya leo.”

Copyright information for SwhNEN