Isaiah 37:8-38
8 aJemadari wa jeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alirudi, akamkuta mfalme akipigana na Libna.9 bBasi Senakeribu akapata taarifa kwamba Tirhaka, Mkushi mfalme wa Misri, alikuwa anaenda kupigana naye. Aliposikia jambo hili akatuma wajumbe kwa Hezekia na neno hili: 10 c“Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usikubali huyo Mungu unayemtumainia akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’ 11 dHakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wametenda kwa nchi zote, wakiwaangamiza kabisa. Je, wewe utaokolewa? 12 eJe, miungu ya mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliweza kuwaokoa? Yaani miungu ya Gozani, Harani, Resefu, na ya watu wa Edeni waliokuwa Telasari? 13 fYuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au wa Iva?”
Maombi Ya Hezekia
14 gHezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la Bwana, akaikunjua mbele za Bwana. 15 hNaye Hezekia akamwomba Bwana akisema: 16 i“Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi. 17 jTega sikio, Ee Bwana, usikie; fungua macho yako, Ee Bwana, uone; sikiliza maneno yote ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.18 k“Ni kweli, Ee Bwana, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya yote pamoja na nchi zao. 19 lWameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu, iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. 20 mSasa basi, Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili kwamba falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee Bwana, ndiwe Mungu.”
Kuanguka Kwa Senakeribu
(2 Wafalme 19:20-37)
21 nKisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Kwa sababu umeniomba kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru, 22 ohili ndilo neno ambalo Bwana amelisema dhidi yake:“Bikira binti Sayuni anakudharau na kukudhihaki.
Binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake unapokimbia.
23 pNi nani uliyemtukana na kumkufuru?
Ni nani uliyeinua sauti yako dhidi yake,
na kumwinulia macho yako kwa kiburi?
Ni dhidi ya yule Aliye Mtakatifu wa Israeli!
24 qKupitia kwa wajumbe wako
umelundika matukano juu ya Bwana.
Nawe umesema,
‘Kwa magari yangu mengi ya vita,
nimepanda juu ya vilele vya milima,
vilele vya juu sana katika Lebanoni.
Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu,
misunobari yake iliyo bora sana.
Nimefikia sehemu zake zilizoinuka juu sana,
misitu yake iliyo mizuri sana.
25 rNimechimba visima katika nchi za kigeni
na kunywa maji yake.
Kwa nyayo za miguu yangu
nimekausha vijito vyote vya Misri.’
26 s“Je, hujasikia?
Zamani sana niliamuru hili.
Siku za kale nilipanga hili;
sasa nimelifanya litokee,
kwamba umegeuza miji yenye ngome
kuwa malundo ya mawe.
27 tWatu wa miji hiyo wameishiwa nguvu,
wanavunjika mioyo na kuaibishwa.
Wao ni kama mimea katika shamba,
kama machipukizi mororo ya kijani,
kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba,
ambayo hukauka kabla ya kukua.
28 u“Lakini ninajua mahali ukaapo,
kutoka kwako na kuingia kwako,
na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu.
29 vKwa sababu unaghadhibika na ufidhuli dhidi yangu,
na kwa sababu ufidhuli wako umefika masikioni mwangu,
nitaweka ndoana yangu puani mwako
na hatamu yangu kinywani mwako,
nami nitakufanya urudi kwa njia ile uliyoijia.
30 w“Hii ndiyo itakuwa ishara kwako, ee Hezekia:
“Mwaka huu utakula kile kiotacho chenyewe,
na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake.
Lakini katika mwaka wa tatu panda na uvune,
panda mashamba ya mizabibu na ule matunda yake.
31 xMara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda
wataeneza mizizi chini na kuzaa matunda juu.
32 yKwa kuwa kutoka Yerusalemu watakuja mabaki,
na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika.
Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote,
ndio utatimiza jambo hili.
33 z“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana kuhusu mfalme wa Ashuru:
“Hataingia katika mji huu
wala hatapiga mshale hapa.
Hatakuja mbele yake na ngao
wala kupanga majeshi kuuzingira.
34 aaKwa njia ile aliyoijia ndiyo atakayorudi;
hataingia katika mji huu,”
asema Bwana.
35 ab“Nitaulinda mji huu na kuuokoa,
kwa ajili yangu mwenyewe,
na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu!”
36 acNdipo malaika wa Bwana akaenda, akawaua wanajeshi 185,000 katika kambi ya Waashuru. Wenzao walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali! 37 adBasi Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Akarudi Ninawi na kukaa huko.
38 aeSiku moja, alipokuwa akiabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza wakamuua kwa upanga, nao wakakimbilia nchi ya Ararati. Naye Esar-Hadoni mwanawe akawa mfalme badala yake.
Copyright information for
SwhNEN