‏ Luke 15:11-32

Mfano Wa Mwana Mpotevu

11 aYesu akaendelea kusema: “Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. 12 bYule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake.

13 c “Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokuwa navyo, akaenda nchi ya mbali, na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa. 14Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana chochote. 15 dKwa hiyo akaenda akaajiriwa na mwenyeji mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. 16 eAkatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa chochote.

17 “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa! 18 fNitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. 19Sistahili tena kuitwa mwanao; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’ 20 gBasi akaondoka, akaenda kwa baba yake.

“Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.

21 h “Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’

22 i “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake. 23Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. 24 jKwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena; alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.

25 “Wakati huo, yule mwana mkubwa alikuwa shambani. Alipokaribia nyumbani, akasikia sauti ya nyimbo na watu wakicheza. 26Akamwita mmoja wa watumishi na kumuuliza, ‘Kuna nini?’ 27Akamwambia, ‘Ndugu yako amekuja, naye baba yako amemchinjia ndama aliyenona kwa sababu mwanawe amerudi nyumbani akiwa salama na mzima.’

28 k “Yule mwana mkubwa akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi baba yake akatoka nje na kumsihi. 29Lakini yeye akamjibu baba yake, ‘Tazama! Miaka yote hii nimekutumikia na hata siku moja sijaacha kutii amri zako, lakini hujanipa hata mwana-mbuzi ili nifurahi na rafiki zangu. 30 lLakini huyu mwanao ambaye ametapanya mali yako kwa makahaba aliporudi nyumbani, wewe umemchinjia ndama aliyenona!’

31 m “Baba yake akamjibu, ‘Mwanangu, umekuwa nami siku zote na vyote nilivyo navyo ni vyako. 32 nLakini ilitubidi tufurahi na kushangilia kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa na sasa yu hai; alikuwa amepotea naye amepatikana.’ ”

Copyright information for SwhNEN