Numbers 8:6-22
6 a“Watwae Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli wengine na uwatakase kwa kawaida ya ibada. 7 bIli kuwatakasa fanya hivi: Nyunyizia maji ya utakaso juu yao; kisha uwaambie wanyoe nywele kwenye mwili mzima, wafue nguo zao na hivyo wajitakase wenyewe. 8 cWaambie wamchukue fahali mchanga pamoja na sadaka yake ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kisha utamchukua fahali mchanga wa pili kwa ajili ya sadaka ya dhambi. 9 dWalete Walawi mbele ya Hema la Kukutania na ukusanye jumuiya yote ya Waisraeli. 10 eUtawaleta Walawi mbele za Bwana, na Waisraeli wataweka mikono yao juu ya Walawi. 11 fAroni atawaweka Walawi mbele za Bwana kama sadaka ya kuinua kutoka kwa Waisraeli, ili kwamba wawe tayari kuifanya kazi ya Bwana.12 g“Baada ya Walawi kuweka mikono yao juu ya vichwa vya hao mafahali wawili, tumia mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi kwa Bwana, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi. 13 hWaambie hao Walawi wasimame mbele ya Aroni na wanawe, kisha wawatoe kama sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana. 14 iKwa njia hii utakuwa umewatenga Walawi kutoka kwa Waisraeli wengine, nao Walawi watakuwa wangu.
15 j“Utakapokuwa umekwisha kuwatakasa Walawi na kuwatoa kama sadaka ya kuinuliwa, watakuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania. 16 kWao ndio Waisraeli ambao watatolewa kabisa kwangu. Nimewatwaa kama mali yangu mwenyewe badala ya mzaliwa wa kwanza, mzaliwa wa kwanza wa kiume kutoka kwa kila mwanamke wa Kiisraeli. 17 lKila mzaliwa wa kwanza wa kiume katika Israeli, awe wa mwanadamu au mnyama, ni wangu. Wakati nilipowaua wazaliwa wote wa kwanza huko Misri, niliwatenga kwa ajili yangu mwenyewe. 18 mNami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wote wa kwanza wa kiume katika Israeli. 19 nKati ya Waisraeli wote, nimempa Aroni na wanawe Walawi kama zawadi ili wafanye kazi katika Hema la Kukutania kwa niaba ya Waisraeli, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili pasiwepo na pigo lolote litakalowapata Waisraeli wakati watakapokaribia mahali patakatifu.”
20Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawafanyia Walawi kama Bwana alivyomwamuru Mose. 21 oWalawi wakajitakasa wenyewe na wakafua nguo zao. Kisha Aroni akawasogeza mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa. 22 pBaada ya hayo, Walawi walikuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania chini ya usimamizi wa Aroni na wanawe. Waliwafanyia Walawi kama vile Bwana alivyomwamuru Mose.
Copyright information for
SwhNEN