‏ 1 Chronicles 21

Daudi Ahesabu Wapiganaji

(2 Samweli 24:1-25)

1 aShetani akainuka dhidi ya Israeli na kumshawishi Daudi ahesabu watu wa Israeli. 2 bKwa hiyo Daudi akamwambia Yoabu na majemadari wa jeshi, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli kuanzia Beer-Sheba mpaka Dani. Kisha nileteeni taarifa ili kwamba niweze kufahamu wako wangapi.”

3Yoabu akajibu, “Bwana na aongeze jeshi lake mara mia na zaidi. Mfalme bwana wangu, kwani hawa wote si raiya wa bwana wangu? Kwa nini bwana wangu unataka kufanya hivi? Kwa nini kuleta hatia juu ya Israeli?”

4 cHata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu; kwa hiyo Yoabu akaondoka na kuzunguka Israeli yote kisha akarudi Yerusalemu. 5Yoabu akampa Daudi jumla ya idadi ya watu wanaoweza kupigana. Katika Israeli kulikuwa na watu 1,100,000 ambao wangeweza kutumia upanga na katika Yuda watu 470,000.

6 dLakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme. 7Amri hii ilikuwa mbaya machoni pa Mungu pia; hivyo akaiadhibu Israeli.

8 eKisha Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Sasa, ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”

9 f Bwana akamwambia Gadi, mwonaji wa Daudi, 10“Nenda ukamwambie Daudi, hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ”

11Kwa hiyo Gadi akamwendea Daudi akamwambia, “Hili ndilo Bwana asemalo: ‘Chagua: 12 gmiaka mitatu ya njaa, au miezi mitatu ya kushindwa na adui zako, ukipatwa na upanga wao, au siku tatu za upanga wa Bwana, yaani, siku tatu za tauni katika nchi na malaika wa Bwana akiangamiza kila mahali katika Israeli.’ Sasa basi, amua jinsi nitakavyomjibu yeye aliyenituma.”

13 hDaudi akamwambia Gadi, “Ninayo mahangaiko makubwa. Mimi na nianguke mikononi mwa Bwana kwa maana rehema zake ni kuu mno, lakini usiniache niangukie mikononi mwa wanadamu.”

14 iBasi Bwana akatuma tauni katika Israeli, watu 70,000 wa Israeli wakafa. 15 jMungu akapeleka malaika kuangamiza Yerusalemu. Lakini malaika alipokuwa akifanya hivyo, Bwana akaona na akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anaangamiza watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Bwana alikuwa amesimama katika sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna
Pia anaitwa Ornani kwa Kiebrania.
Myebusi.

16 lDaudi akayainua macho yake akamwona huyo malaika wa Bwana akiwa amesimama katikati ya mbingu na dunia, naye ameunyoosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuangamiza. Kisha Daudi na wazee, waliokuwa wamevaa nguo za gunia, wakaanguka kifudifudi.

17 mDaudi akamwambia Mungu, “Je, si mimi ndiye niliyeamuru watu wahesabiwe? Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Ee Bwana, Mungu wangu, mkono wako na uwe juu yangu mimi na jamaa yangu, lakini usiache tauni hii iendelee juu ya watu wako.”

18Kisha malaika wa Bwana akamwamuru Gadi amwambie Daudi apande na kumjengea Bwana madhabahu kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi. 19Kwa hiyo Daudi akakwea, akalitii lile neno ambalo Gadi alikuwa amelisema katika jina la Bwana.

20 nArauna alipokuwa akipura ngano, akageuka akamwona yule malaika. Wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha, yeye akaendelea kupura ngano. 21Kisha Daudi akakaribia, Arauna alipotazama na kumwona, akaondoka kwenye uwanja wa kupuria nafaka akamsujudia Daudi akiuinamisha uso wake ardhini.

22 oDaudi akamwambia, “Nipatie huu uwanja wako wa kupuria nafaka ili niweze kujenga madhabahu ya Bwana tauni ipate kukomeshwa katika watu. Niuzie kwa bei yake kamili.”

23Arauna akamwambia Daudi, “Uchukue huo uwanja. Mfalme bwana wangu na afanye lolote analopenda. Tazama, nitatoa maksai kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, vifaa vya kupuria kuwa kuni, pamoja na ngano kwa ajili ya dhabihu ya nafaka. Natoa hivi vyote.”

24Lakini Mfalme Daudi akamjibu Arauna, “La hasha! Lakini ninasisitiza kwamba nitalipa bei yake kamili. Sitachukua kilicho chako kwa ajili ya Bwana au kutoa sadaka ya kuteketezwa ambayo hainigharimu chochote.”

25 pBasi Daudi akamlipa Arauna shekeli za dhahabu 600
Shekeli 600 za dhahabu ni sawa na kilo 7.
kwa ajili ya ule uwanja.
26 rKisha Daudi akamjengea Bwana madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Akamwita Bwana naye Bwana akajibu maombi yake kwa moto toka mbinguni juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.

27Kisha Bwana akanena na yule malaika, naye akarudisha upanga wake katika ala yake. 28Wakati huo, Daudi alipoona kwamba Bwana amemjibu kule kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna Myebusi, akatoa dhabihu huko. 29 sMaskani ya Bwana ambayo Mose aliitengeneza kule jangwani, pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa wakati huo vilikuwa viko mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni. 30 tLakini Daudi hakuthubutu kuisogelea ili kumuuliza Mungu, kwa sababu aliuogopa upanga wa yule malaika wa Bwana.

Copyright information for SwhNEN