Judges 19
Mlawi Na Suria Wake
1 aKatika siku hizo Israeli hawakuwa na mfalme.Basi Mlawi mmoja aliyeishi sehemu za mbali katika nchi ya vilima ya Efraimu, akamchukua suria mmoja kutoka Bethlehemu ya Yuda. 2Lakini suria wake akafanya ukahaba dhidi yake, naye akamwacha akarudi nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu ya Yuda. Baada ya kukaa huko kwa muda wa miezi minne, 3mume wake akaenda kumsihi ili arudi. Alikwenda na mtumishi wake na punda wawili. Yule mwanamke akamkaribisha nyumbani mwa baba yake, baba yake alipomwona akamkaribisha kwa furaha. 4 bBaba mkwe wake, yaani, baba yake yule msichana, akamzuia ili akae, hivyo akakaa na huyo baba mkwe wake kwa siku tatu, wakila, wakinywa na kulala huko.
5 cSiku ya nne wakaamka mapema naye akajiandaa kuondoka, lakini baba wa yule msichana akamwambia mkwewe, “Ujiburudishe kwa kula kitu chochote, ndipo uweze kwenda.” 6 dBasi wakaketi wote wawili ili kula na kunywa pamoja. Baadaye baba wa msichana akamwambia, “Tafadhali ubakie usiku huu upate kujifurahisha nafsi yako.” 7Basi yule mtu alipotaka kuondoka baba wa yule msichana akamsihi, basi akabaki usiku ule. 8Asubuhi ya siku ya tano, alipoamka ili aondoke, baba wa yule msichana akamwambia, “Jiburudishe nafsi yako. Ngoja mpaka mchana!” Kwa hiyo wote wawili wakala chakula pamoja.
9Basi wakati yule mtu alipoinuka aende zake, pamoja na suria wake na mtumishi wake, baba mkwe wake, yaani, baba wa yule msichana akamwambia, “Tazama sasa jioni inakaribia. Ulale hapa usiku unakaribia. Ukae, ukajifurahishe nafsi yako. Kesho unaweza kuamka mapema asubuhi na uende nyumbani kwako.” 10 eLakini akakataa kulala tena, akaondoka na kwenda mpaka Yebusi (ndio Yerusalemu), akiwa na punda wake wawili waliotandikiwa, pamoja na suria wake.
11 fAlipokaribia Yebusi na usiku ukiwa umekaribia, mtumishi akamwambia bwana wake, “Haya sasa natuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo.”
12Lakini bwana wake akamjibu, “Hapana. Hatutaingia kwenye mji wa kigeni, ambao watu wake si Waisraeli. Tutaendelea mpaka tufike Gibea.” 13 gAkasema, “Haya, tujitahidi tufike Gibea au Rama, nasi tutalala katika mji mmojawapo.” 14 hHivyo wakaendelea na safari, jua likachwea walipokaribia Gibea ambao ni mji wa Benyamini. 15 iWakageuka ili kuingia na kulala Gibea. Wakaingia humo, wakaketi kwenye uwanja wa mji, wala hakuna mtu yeyote aliyewakaribisha kwake ili wapate kulala.
16 jJioni ile mtu mmoja mzee toka nchi ya vilima ya Efraimu, aliyekuwa anaishi huko Gibea (watu wa sehemu ile walikuwa Wabenyamini), akarudi kutoka kwenye kazi za shamba. 17 kAlipotazama na kuwaona hao wasafiri katika uwanja wa mji, yule mzee akawauliza, “Ninyi mnakwenda wapi? Nanyi mmetoka wapi?”
18 lAkamwambia, “Tumepita kutoka Bethlehemu ya Yuda, tunaelekea katika nchi ya vilima ya Efraimu, ambako ndiko ninakoishi. Nilikwenda Bethlehemu ya Yuda na sasa ninakwenda katika nyumba ya Bwana. Hakuna mtu yeyote aliyenikaribisha katika nyumba yake. 19 mTunazo nyasi na chakula cha punda wetu na mkate na divai kwa ajili yetu sisi watumishi wako, yaani mimi, mtumishi wako mwanamke, pamoja na huyu kijana tuliyefuatana naye. Hatuhitaji kitu chochote.”
20Yule mzee akawaambia, “Amani iwe kwenu! Karibuni nyumbani mwangu. Nitawapa mahitaji yenu yote, msilale katika uwanja huu wa mji.” 21 nHivyo akamwingiza nyumbani mwake na kuwalisha punda wake. Baada ya kunawa miguu yao, wakala na kunywa.
22 oWalipokuwa wakijiburudisha, watu waovu wa mji huo, wakaizingira ile nyumba. Wakagonga mlango na kusema na yule mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mtu aliyeingia kwako, tupate kumlawiti.”
23 pYule mwenye nyumba akatoka nje na kuwaambia, “Hapana, ndugu zangu msiwe waovu namna hii, ninawasihi. Kwa kuwa huyu mtu ni mgeni wangu msifanye jambo hili la aibu. 24 qTazameni, hapa yupo binti yangu ambaye ni bikira na suria wa huyu mtu. Nitawatoleeni hawa sasa, mkawatwae kwa nguvu na kuwafanyia lolote mtakalo. Lakini kwa mtu huyu msimfanyie jambo ovu hivyo.”
25 rLakini wale watu hawakumsikia. Hivyo yule mtu akamtoa yule suria wake nje kwa wale watu, nao wakambaka na kumnajisi usiku ule kucha mpaka asubuhi. Kulipoanza kupambazuka wakamwachia aende. 26Alfajiri yule mwanamke akarudi kwenye ile nyumba bwana wake alikokuwa, akaanguka chini mlangoni, akalala pale hata kulipopambazuka.
27Bwana wake alipoamka asubuhi na kufungua mlango wa nyumba na kutoka nje ili kuendelea na safari yake, tazama, yule suria wake alikuwa ameanguka pale penye ingilio la nyumba na mikono yake ikiwa penye kizingiti cha chini. 28Akamwambia yule suria, “Inuka, twende.” Lakini hakujibu. Yule bwana akamwinua akampandisha juu ya punda wake, wakaondoka kwenda nyumbani.
29 sAlipofika nyumbani, akachukua kisu na kumkatakata yule suria kiungo kwa kiungo, sehemu kumi na mbili, na kuvipeleka hivyo vipande katika sehemu zote za Israeli. 30 tKila mtu aliyeona akasema, “Jambo la namna hii halijaonekana wala kutendeka, tangu Israeli walipopanda kutoka Misri. Fikirini juu ya jambo hili! Tafakarini juu ya jambo hili! Tuambieni tufanye nini!”
Copyright information for
SwhNEN